Monday, May 31, 2010

Mwalimu na mwanafunzi wake

Tembelea http://mawaidha.info

Baada ya kumsomesha muda usiopungua miaka 30, Sheikh alimuuliza mwanafunzi wake:
"Umejifunza nini kutoka kwangu miaka yote hii?"
Mwanafunzi akajibu:
"Kusema kweli sikujifunza isipokuwa machache tu."
Sheikh akasema kwa mshangao:
"Nimekusomesha muda wa miaka 30, kisha unaniambia hukujifunza isipokuwa machache tu! Haya nielezee hayo machache ni yepi?"
Mwanafunzi akasema:
"Niliuangalia ulimwengu, nikaona kila kitu kinmahitajia wa kukiendesha. Kisha nikawaaangalia wanadamu, nikawaona wanawategemea wengine wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Na nilipofahamu kutoka kwako ewe ustadhi wangu kuwa hapana kinachoweza kuwepo bila ya Mwenyezi Mungu kutaka, nikaacha kumtegemea ye yote isipokuwa Mwenyezi Mungu."

Sheikh akasema:
"Enhe? Endelea."
Mwanafunzi akasema:
"Kisha nikawaangalia viumbe. Nikaona kila mmoja ana kipenzi chake. Wanaishi pamoja, wanacheza, wanasafiri na kurudi pamoja katika safari zao zote. Lakini katika safari ile ya mwisho, mtu anapowasili kaburini pake, anaingia kule ndani peke yake, na vipenzi vyake vyote vinabaki nje. Hawawezi kumfuata. Nikaona bora nijaalie kipenzi changu kiwe amali zangu njema ili ziwe pamoja nami nitakapokuwa kaburini peke yangu."

Sheikh akasema:
"Ahsante! Ehe? Endelea."
Mwanafunzi akasema:
"Kisha nikawaangalia wanadamu. Nikawaona kila mmoja pesa ikishaingia mkononi mwake haitoki. Watu wake wenye shida hawapati haki zao. Masikini hawapati haki zao. Kisha nikatafakari juu ya maneno ya Mwenyezi Mungu katika Suratul Nahl aya ya 96 isemayo:
مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللّهِ بَاقٍ
"Mlivyonavyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu (vya jaza yenu) ndivyo vitavyobakia."

Nikawa kila kinachoingia mikononi mwangu hukitoa ili kipate kubaki huko kwa Mwenyezi Mungu."

Kwa kukifafanua zaidi kifungu hiki, tuangalie namna gani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alivyokuwa akitoa.
Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) baada ya kuchinja mbuzi na kuigawa nyama yote alimuuliza Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) kama bado pana chochote kilichosalia. Bibi Aisha akasema:
"Limebaki hili bega tu."
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akamsahihisha kwa kumuambia:
"Bali ile tuliyoigawa ndiyo iliyobaki ewe Aisha."

Katika hadithi nyingine, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:
"Kipo kingine unachofaidika nacho katika mali yako isipokuwa kile unachokula kikaoza tumboni na unachokivaa kikachakaa na unachotoa sadaka kikabaki?"

Sheikh akasema:
"Enhe, endelea."
Mwanafunzi akasema:
"Nikawatizama viumbe. Nikawaona kila mmoja anamuonea husuda mwenzake kwa kile alichokipata. Nikakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu katika Suratul Zukhruf aya ya 32 yasemayo:
أَهُمْ يَقْسِمُونَ رَحْمَةَ رَبِّكَ نَحْنُ قَسَمْنَا بَيْنَهُم مَّعِيشَتَهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَرَفَعْنَا بَعْضَهُمْ فَوْقَ بَعْضٍ دَرَجَاتٍ
"Je, wao wanaigawa rehema ya Mola wako (wakampa wampendae na kumnyima wamtakae?) Sisi tumewagawiya maisha yao katika uhai wa dunia na kuwainua baadhi yao daraja kubwa juu ya wengine."

"Nikaacha kuwahusudu viumbe”.
Sheikh akasema:
"Ahsante. Endelea."
Mwanafunzi akasema:
"Kisha nikawatizama wanadamu. Nikaona tonge imewadhalilisha na kuwafanya wapige mbizi katika mambo ya haramu. Nikakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu katika Surat Hud aya ya 6 ِAliposema:
وَمَا مِن دَآبَّةٍ فِي الأَرْضِ إِلاَّ عَلَى اللّهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ
"Na hakuna kiumbe cho chote katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Mwenyezi Mungu. Na anajua makao yake ya milele na mahali pake pa kupita tu.Yote yamo katika kitabu kinachodhihirisha (kila kitu)."

Nikafahamu kuwa riziki yangu hawezi kuichukua mwengine, na hapo moyo wangu ukatulia. "

Katika kukisherehesha kifungu hiki tuzingatie maneno ya Hassan Al-Basri (Radhiya Llahu anhu) mmoja katika Maulamaa wa At-Tabiina. (waliowaona Masahaba (Radhiya Llahu anhum) lakini hawakumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam).
Hassan Al Basri alisema:
"Nilipotambua kuwa amali zangu hawezi kunifanyia mwengine, nikapania kuzifanya mwenyewe. Na nilipotambua kuwa riziki yangu hawezi kuichukuwa mwengine, moyo wangu ukatulia. Na nilipotambua kuwa Mola wangu ananiona, nikaona haya asije akaniona nikiwa katika hali ya kumuasi.”

Wasalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

No comments:

Post a Comment