Monday, May 31, 2010

Waliopata vitambulisho vya ukaazi washindwa kujiandikisha DKWK Z`bar


Wanzanzibari 99,047 waliopata vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi, hawajajitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) visiwani hapa.

Mkurugenzi wa idara ya usajili wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohammed Juma Ame, alisema hayo wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri mjini hapa mwishoni mwa wiki.

Alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, jumla wa watu 408,178 wamesajiliwa katika DKWK ilipofika Mei 9, mwaka huu.

Aidha, alisema Wazanzibari 562,008 wameshapewa vitambulisho hivyo tangu usajili huo ulipoanza mwaka 2005.

Ame alisema kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), idadi ya watu waliotarajiwa kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni 500,000.

Ame alisema ipo haja yakufanya utafiti ili kujua sababu za watu waliopata vitambulisho vya kudumu, kutojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura.

“Idadi ya watu waliopata vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi, wakashindwa kujiorodhesha kwa ajili ya kupiga kura ni kubwa, haiwezekani wawe wamehama Zanzibar au kufa,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja kwa taasisi zinazohusika kufanya utafiti wa kina ili kubaini sababu zake.

Hata hivyo alisema Wazanzibari wengi wameanza kuchoshwa na ahadi za wanasiasa, na kuamua kutojiakishaji kupiga kura.

“Zanzibar watu wameanza kuchoshwa na ahadi za wanasiasa na kuamua kutojitokeza kuandikishwa kuwa wapiga kura, licha ya kwamba wana vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi,” alisema.

Hata hivyo, alisema uchunguzi walioufanya ulibaini kuwa baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa (masheha) wanajihusisha na urasimu katika utoaji wa fomu za kuwawezesha kupata vitambulisho.

Alisema urasimu huo unafanyika kwa visingizio vya kuishiwa fomu, na wengine (masheha) wanatoza fedha ili kutoa barua za usajili.

Ame alisema idara yake imeanza kuwaorodhesha masheha wenye tabia hiyo, ili waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

Alisema kuanzia Desemba, 2009 hadi Mei mwaka huu, ofisi ya usajili wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, ilipokea rufaa 515, 405 kati ya hizo zilitoka Unguja wakati 110 zilitoka Pemba. Zote zimefanyiwa kazi.

Hata hivyo alisema kwamba idadi kubwa ya rufaa za Pemba zilionyesha kuwa wahusika walishindwa kupata vitambulisho kutokana na kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa.

Alisema wengi wao walionyesha kadi za kliniki badala ya cheti kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi huyu alisema Machi 23, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, aliwasilisha malalamiko mapya kwa Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume, na kukabidhi orodha ya watu 3,235 waliodai kunyimwa vitambulisho, lakini baada ya uchunguzi, madai hayo yalionekana si ya kweli.

Hata hivyo alisema baada ya orodha hiyo kuhakikiwa, ilibainika kuwa watu 2,018 wamesajiliwa tangu 2005, lakini wameshindwa kuchukua vitambulisho vyao katika ofisi za usajili za wilaya zilizopo Unguja na Pemba.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment