Monday, May 31, 2010
Wabunge watano hoi kura ya maoni
WABUNGE watano na mwakilishi wawili wamebwagwa na hivyo kupoteza nafasi ya kusimama kutetea nafasi zao kwenye uchaguzi mkuu ujao baada ya kumalizika kura za maoni ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), kisiwani Pemba.Wabunge hao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mwakilishi mmoja wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar hawatashiriki katika uchaguzi mkuu wa 2010 baada ya kuanguka katika hatua hiyo ya mwanzo kisiwani Pemba ambako CUF ina nguvu kubwa.
Katiba ya CUF imerudisha mamlaka ya kuteua wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kwa wananchi majimboni mwao ili kuamua nani anawafaa kuwawakilisha katika uchaguzi mkuu.
Habari kutoka kwa makatibu wa CUF wa wilaya na majimbo zinawataja wabunge walioanguka kuwa ni Omar Ali Mzee wa jimbo la Kiwani wilaya ya Mkoani, Juma Said Omar (Mtambwe, Wete), Salim Yussuf Mohammed (Kojani), Mwadini Abbas Jecha (Wete).
Wengine ni Fatma Maghimbi wa Chakechake Wilaya ya Chakechake.
Wawakilishi walioanguka Muhidin Mohamed Muhidin wa Mtambile na mwakilishi wa jimbo la Chambani Wilaya ya Mkoani, Abbas Juma Mhunzi.
Katibu wa Wete, Mkoa wa kaskazini, Maulid Khalid alisema katika jimbo hilo mbunge wa sasa Mwadini Abbass Jecha alimanguka baada ya kuambulia kura 255.
“Mbarouk Salum alishinda katika kura ya maoni ya ubunge wa jimbo la Wete baada ya kupata kura 885 na kuwaangusha wagombea wengine sita,” alisema Khalid.
Wagombea wengine ni Mohammed Khalfan (500), Ali Jabir (300), Kombo Hamis (186), Hamad Issa (110) na Seif Azzan (90).
Kwa upande uwakilishi, Khalid alisema Asaa Othman Hamad ambaye ni mwakilishi wa sasa, alifanikiwa kurudi kwa kupata kura 1,300. Khalid alisema wagombea wengine walioshiriki katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya chama katika nafasi ya uwakilishi ni Harif Said (407), Maryam Abdallah (397), Issa Rubea (130) na Masoud Hamad (50).
“Kura zote kwa jimbo langu zilikuwa 2,300 na kura 70 ziliharibika,” alisema Khalid.
Katibu wa CUF wa Jimbo la Kojani, Nassor Ali Othman aliliambia Mwananchi jana kwa njia ya simu kuwa Salim Yussuf Mohammed alipoteza nafasi ya kutetea kiti hicho baada ya kuambulia 355 wakati mshindi, Rashid Ali Omar alizoa kura 1,130.
Othmani alisema wagombea wa ubunge katika kura hiyo ya maoni walikuwa Asaa Mkambaya (899), Juma Khamis (437), Ghalib Mohammed (224), Haji Mussa (168), Hamad Bakar (158), Hamad Omar (138), Salim Hamad (71) na Omar Juma kura 38.
“Kura zote kwa upande wa ubunge zilikuwa 3696 wakati kura 77 ziliharibika. Kwa upande wa uwakilishi kura zote zilizopigwa zilikuwa 3,704 lakini kwa bahati mbaya kura 411 ziliharibika,” alisema Othman.
Othman alisema kuwa mwakilishi wa zamani, Omar Ali Jadi alishinda baada ya kupata kura 1,204.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa, mwakilishi huyo alimshinda mpinzani wake wa karibu, Hassan Hamad aliyepata 1,192, huku Ali Mjaa Ali akiambulia kura 504 na Salim Bakar Salim (393).
Katibu wa jimbo la Mtambwe, Seif Massoud Sheha aliliambia Mwananchi kuwa mbunge wa sasa, Juma Said Omar aliangushwa na Said Suleiman Said aliyepata kura 693.
“Kwa upande wa ubunge tulikuwa na jumla ya wagombea 12 na uwakilishi wagombea saba. Kura zote kwa ubunge zilikuwa 2,403 lakini kura 47 ziliharibika,” alisema Sheha.
Kwa mujibu wa Sheha, Said Suleiman Said alipata kura 693, Mohammed Hamad Osama' (387), mbunge wa sasa, Juma Said Omar (319) na Salim Sheha (231).
Wengine ni Said Masoud (179), Omar Mbarouk (140), Suleiman Mbarouk (127), Rubea Suleiman (107), Seif Masoud (47), Saleh Ali ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo mwa 1995-2000 (43), Abdallah Ali (43) na Salim Mussa Mjaka (15).
Kwa upande wa uwakilishi Sheha alisema mwakilishi wa jimbo hilo Salim Abdallah amechaguliwa kutetea nafasi yake baada ya kupata kura 676.
Wagombea wingine ni Ghalib Amour (446), Ali Said (380), Bakar Ali (284), Mohammed Suleiman (284), Saida Khamis (189) na Abbas Ali kura 87.
Kwenye jimbo la Gando, katibu wa CUF, Khelef Mohammed Khelef alisema mbunge wa sasa, Khalifa Suleiman Khalifa amefanikiwa kurudi kwa kupata kura 800.
Kaimu katibu wa Wilaya ya Mkoani, Makame Khalid Makame alisema kuwa hadi sasa ni majimbo matatu tu katika wilaya yake ambayo yamekamilika.
“Katika majimbo hayo mbunge wa Kiwani, Omar Ali Mzee ameanguka huku mwakilishi wake akifanikiwa kurudi; Chambani mwakilishi ameanguka huku mbunge akifanikiwa kurudi; jimbo la Mkanyageni Mohammed Habib Mnyaa na mwakilishi wake wote wamepita,” alisema Makame.
Wabunge na wawakilishi wengi walioanguka hawakuweza kupatikana jana kuzungumzia matokeo ya kura hizo za maoni.
Lakini mbunge wa Kojani, Salim Yussuf alisema: “Aaah nimeyapokea kama yalivyokuja, sina la kuzungumza zaidi. Wakubwa wenyewe wataangalia kwa sababu katiba yetu inasema baraza kuu la uongozi ndio lenye maamuzi ya mwisho.”
“Lakini kilichotokea….aaa…sikelewi lakini ndio kimetokea,” aliongeza Yussuf ambaye pia alikuwa mwakilishi wa jimbo la Pandani kuanzia 1995 hadi 2005..
Mbunge wa Kiwani, Omar Ali Mzee alisema anakubali matokeo kwa kuwa hayo ndiyo maamuzi ya wananchi ingawa uzawa kutoka kijiji kimoja hadi kingine ulichangia sana yeye kuanguka.
“Unajua kura ndio kura, lakini uzawa umechangia sana mimi kuanguka. Kwa sababu kila kijiji kilitaka mgombea atoke kwao kwa hiyo kura zikagawika sana. Mathalani vijiji vya Kiwani, Kendwa, Mwambe, Chwaka, Nanguji, Mwambe na Mtangani vyote vilikuwa na wagombea,” alisema Mzee.
Kura zinaendelea kupigwa kisiwani humo huku nyingine zikiendelea kuhesabiwa.
SOURCE: MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment